Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kinatarajia kuzindua, mkakati wa kukuza na kukomaza demokrasia kwenye mashina na matawi mkoani humo lengo likiwa ni kukiimarisha chama hicho katika ngazi zote.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na katibu wa chama cha mapinduzi CCM mkoani humo, Jamila Yusuph alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa lengo la mkakati huo ni kukiimarisha chama hicho hasa katika ngazi za mashina.

Mkakati huo utazinduliwa machi 23, na Katibu mkuu wa CCM taifa, Dkt. Bashiru Alli ambao utaenda sambamba na kugawa vitendea kazi, unalenga kukiimarisha chama hicho, hasa baada ya kuingia kwenye mageuzi ya kimuundo katika ngazi za mashina.

“Ikumbukwe tumefanya mabadiliko katika mfumo wa muundo wa mashina ambapo mara ya kwanza tulikuwa na mashina kuanzia watu watano au nyumba kumi, lakini kwa muundo wa sasa tumeona ili kuwa shina kwa vijijini ni kuanzia 30-150, na kwa mijini ni 50-150, hivyo tutatumia mda huo kutoa elimu hiyo”

Aidha, amesema kuwa mkakati huo unazinduliwa sasa baada ya kufanyia kazi changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma kutokana na mabadiliko ya kimfumo, kimuundo na kiuongozi yaliyofanyika na kupelekea kubadilika mfumo wa muundo wa mashina na matawi.

Pia amesema kuwa endapo mambo hayo yatafanyiwa kazi katika mashina, na matawi, basi wanauhakika wa kuibuka kidedea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao, na kuishangaza dunia kwa ushindi mkubwa itakao upata CCM.

Hata hivyo, ameongeza kuwa wameamua kujikita katika mashina kwa sababu huko ndiko wanaamini waliko wanachama wengi na hilo litasaidia kukijenga chama hicho na kuwa imara zaidi.

 

Kundi la Hezbollah lamkosesha usingizi Pompeo
Kansela wa Ujerumani ampigia simu JPM