Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemfukuza mwandishi wa gazeti la mwananchi, Peter Elias katika msafara wa kampeni wa mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli baada ya kuandika habari inayohusu wanachama wa Chadema kunyooshea vidole viwili mgombea huyo alipotaka kuhutubia katika eneo la Uyole, Mbeya.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, mkurugenzi wa mawasiliano wa CCM, Godfrey Chongolo aliliambia gazeti hilo kuwa habari hiyo iliyochapishwa September 28 kwenye kurasa za mbele haikuwa habari inayofaa.

Chongolo alieleza kuwa zilikuwepo habari nyingi zaidi za kuandika kwa kuwa mgombea huyo alifanya mikutano mitano kabla ya mkutano huo hivyo haoni sababu ya mwandishi huyo kuandika habari hiyo, hivyo wameamua kumtoa mwandishi huyo kwenye kikosi cha waandishi wanaoambatana na mgombea huyo.

“Unajua sisi tuko vitani, kwa hiyo unapoiandika kwamba wanachadema walimshangilia kwa kuonyesha vidole viwili juu maana yake ni kwamba hawamkubali mgombea wetu, sasa hapo unawaambia nini Watanzania,” Chongolo anadaiwa kumwambia mwandishi huyo.

Chongolo aliongeza kuwa mwandishi huyo alipaswa kuandika habari yenye ujumbe kuwa “vijana wa Chadema wafanya fujo kwenye mkutano wa kampeni wa Magufuli”.

Tukio hilo linakumbusha mwaka 2010 ambapo mwandishi wa gazeti hilo, Midraj Ibrahim alitimuliwa kwenye msafara wa mgombea urais wa CCM kwa madai ya kuripoti tukio ambalo chama hicho hakikupenda litangazwe.

Uongozi wa Mwananchi umeeleza kusikitishwa na tukio hilo na kudai kuwa hawatakatishwa tamaa bali wataendelea kuwatuma waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuwa wanawagharamia chakula, malazi pamoja na safari kwa mujibu wa ratiba za kampeni. Hata hivyo, uongozi huo umeeleza kuwa kwa kuwa wagombea hubadili ratiba kwa muda mfupi, waandishi hutumia magari yaliyotolewa na vyama husika kwa ajili ya kuwabeba waandishi hao.

 

Roma Adai Hajapata Barua Ya Wimbo Wake Kufungiwa, Awapa Ushauri BASATA
Magufuli Asema Atafuata Nyayo Za Marais Waliomtangulia