Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Mabeyo, ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Jenerali Mabeyo yupo Nchini Afrika Kusini kuhudhuria sherehe za kumuaga Mkuu Majeshi wa Afrika Kusini Jenerali SZ Shoki zilizofanyika kitaifa Jana Mjini Pretoria.
Kuhudhuria sherehe hizi, ni utaratibu uliowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha ushirikiano hususan katika nyanja ya Diplomasia ya Ulinzi (Defence Diplomacy) na Amani katika eneo la nchi za SADC.
Jenerali Mabeyo, amekaribishwa Ubalozini na Balozi Mej. Jen. Gaudence Milanzi (Mst) na watumishi wa Ubalozi ambapo Balozi Milanzi alitoa taarifa fupi ya eneo la uwakilishi kwa Afrika Kusini, Botswana na Falme ya Lesotho.
Balozi Milanzi ameeleza kuwa hali ya uwakilishi inaridhisha kiulinzi na kiusalama, Ubalozi umeendelea kukuza mashirikiano na nchi za eneo la uwakilishi ikiwa ni pamoja na SADC, kwa kufuata miongozo ya sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kuendeleza Diplomasia ya kisiasa na kutekeleza Diplomasia ya uchumi.
Kwa upande wake Jenerali Mabeyo ameelezea ziara yake kwa ujumla nchini Afrika Kusini kuwa imekuwa ni ya mafanikio, na pia kuna mambo kama ambayo kama Mkuu wa Majeshi ameona yanafaa kuigwa ili kuboresha utendaji wa Jeshi la Tanzania.
Jenerali Mabeyo amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amelenga kuendeleza maendeleo ndani na nje ya nchi, mfano katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwelekeo unaelekeza kuimarisha Diplomasia kwa kujenga mahusiano na nchi duniani kwa kuimarisha Diplomasia ya siasa na Diplomasia ya uchumi.
Jenerali Mabeyo amemsihi Balozi na watumishi wa Ubalozi kuhakikisha kuwa wanaielewa na kuisimamia dira ya Diplomasia kama ilivyoainishwa na Rais Samia , ili kuweza kutelekeza majukumu yao kwa wepesi.