Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Cedric Kaze, amesema wanahitaji kushinda mchezo dhidi ya Simba SC Jumapili (Oktoba 23) ili kurudisha mioyo iliyovunjika ya Mashabiki wao baada ya kutolewa kwenye Michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kaze amesema ana imani Young Africans itafanya vizuri katika mchezo huo hiyo kwa sababu inawafahamu vyema wapinzani wao ambao waliwafunga pia katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwezi Agosti.

“Tulichofanya kwanza ni kuwaweka sawa wachezaji kisaikolojia baada ya kupoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Haikuwa rahisi kwa sababu tuliwekeza nguvu nyingi, inabidi watoke kwenye hali hiyo ya masikitiko kwa sababu imeshatokea,”

“Akili zielekezwe kwenye mchezo wa ‘DABI’ ambao mashabiki wanataka kuona timu inarudi kwenye njia nzuri na kuwasahaulisha kilichotokea. Inabidi tuingie katika mchezo huo kwa nguvu nyingi kutafuta alama tatu,” amesema Kaze.

Ameongeza ushindi pekee ndio utawaweka kwenye nafasi nzuri kuelekea michezo wa Ligi Kuu inayofuata pamoja na mchezo wa hatua ya mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain ya Tunisia utakaochezwa Novemba 2, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

60 wapoteza maisha ghasia za kuipinga Serikali
Maandalizi mrithi wa Waziri Mkuu yaanza