Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa hakina imani na maamuzi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai kutangaza kumvua ubunge mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama hicho, Tundu Lissu.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mambo ya Nje wa Chama hicho, John Mrema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa maamuzi hayo hayajafuata utaratibu ambao unafahamika katika bunge.
Amesema kuwa Lissu alikuwa mahtuti kipindi anaondoka kwenda kwenye matibabu, hivyo asingeweza kuandika barua bali spika alitakiwa kuangalia mazingira halisi aliyokuwa nayo mbunge huyo.
”Hii inashangaza sana, kuomba barua ya Lissu kwenda kutibiwa wakati akiwa mtu yuko mahtuti, kwakweli hili tutalisimamia kisheria kuhusu kufukuzwa kwa Lissu, lazima twende mahakamani kudai haki yetu ya msingi kwa Lissu, jambo hili tumelidhibiti na tuko sawa,”Amesema Mrema
Hata hivyo, hivi karibuni, Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai alitangaza kumvua nafasi ya ubunge Tundu Lissu mara baada ya kwenda kinyume na taratibu za bunge ambazo kisheria vinabariki kuvuliwa ubunge kwa mbunge huyo.