Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakiongozwa na Tundu Lissu, wanatarajiwa kuongeza nguvu kwenye mashauri manne ya uchochezi yanayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema.
Lissu amesema kuwa Chadema pia wanatarajia kuviandika barua vyama vya kitaalamu vya wanasheria kikiwemo kile cha Tanganyika, (TLS) na kile cha Afrika Mashariki(EACJ) ili vitoe msimamo wao endapo vinapinga dhamana ya Lema lilivyoshughulikiwa mahakamani hapo.
Lema yuko mahabusu kwa siku 72 sasa tokea alipokamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma na kupelekwa Jijini Arusha kwaajili ya mahojiano.
“Tunawataka walaani vile vitendo vya ukiukwaji wa wazi wa sheria na wanachama wetu walio Arusha ambao hawahitaji kupanda ndege kufika mahakamani kuungana nasi katika kuhakikisha haki inapatikana mahakamani, kwakuwa mahakama inazuia wananchi wa kawaida kuingia mahakamani siku kesi za Lema zinapokuja mahakamani, tumeamua kuleta mawakili wengi waje kujaa mahakamani, tunataka kesi hizi ziwe na kelele kubwa itakayovunja ukuta wa magereza,” amesema Lissu.
Kwa upande wa mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe,ameitupiwa lawama serikali kwa kusema kuwa ina mkono katika sakata la Lema ndiyo maana anazidi kusota mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili na nusu sasa.