Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, Tumaini Makene amesema kuwa madiwani wa Halmashauri ya Ubungo hawajagomea mkutano wa baraza hilo bali wamehisi kuna mchezo mchafu unaofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kushindwa kumuapisha Diwani wa viti maalum.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na EATV, ambapo Makene amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha anaondoa vikwazo na kumuapisha Diwani huyo, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa anakiuka maagizo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwani ndiyo iliyomteua Diwani huyo wa Viti Maalumu, Anna Kajigiri .
”Walitarajia katika kikao hicho kwa mujibu wa ratiba Anna Kajigiri ataapishwa kuwa sehemu ya baraza, sasa madiwani wenzake wanahisi kuna mchezo mchafu unafanyika kwenye ofisi ya Mkurugenzi, kutomuapisha tofauti na maelekezo ya NEC ambayo imemteua Anna Kajigiri kuwa Diwani halali wa Halmashauri ya Ubungo, kimsingi hawajagomea mkutano isipokuwa waameeleza wasiwasi wao dhidi ya uzembe wa ofisi ya Mkurugenzi kushindwa kumthibitisha mwenzao kuwa diwani,”amesema Makene.
Kufuatia hali hiyo CHADEMA imemuomba Mkurugenzi huyo kumuapisha Diwani wao na kwamba yeye kama Mtumishi wa Umma si vyema kuweka mbele masuala ya kisiasa na kukiuka maagizo ya NEC, chombo ambacho kina mamlaka ya mwisho ya kumtangaza nani anafaa kuwa Diwani au Mbunge.