Ungozi wa Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) umesema kwa kiwango cha fedha walichokipata hadi sasa wanaanza mchakato wa kuwatoa gerezani viongozi wao wanawake.
Mkurugenzi wa itikadi, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema mawakili wa chama hicho wameanza kufuatilia namba ili kulipa faini ya milioni 110 inayotakiwa kulipwa na wabunge wanawake watatu, Halima Mdee, Easter Bulaya, Easter Matiko.
Viongozi nane wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, jana walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, kulipa faini ambayo ni zaidi ya Shilingi Milioni 350, au kifungo cha miezi mitano jela.
Leo asubuhi wanachama wa Chama cha mapinduzi CCM, wakiongozwa na katibu wa itikadi na uenezi Humphrey Polepole, wamefanikiwa kumlipia faini ya sh. milioni 30, mwanachama wao mpya dkt. Vicent Mashinji na wameongozana kwenda Gereza la Segerea ili kukamisha utaratibu wa kumtoa.