Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza hatua inayofuata baada ya wabunge wake kumaliza siku 14 za kukaa karantini kwa lengo la kujitathmini kiafya dhidi ya maambukizi ya virusi vipya vya corona (covid-19).
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amesema leo, Mei 15, 2020 wabunge wake wanatarajia kurejea bungeni kwani wamekamilisha siku hizo.
“Wabunge wetu wote ambao walitekeleza makubaliano na uamuzi wa chama wa kujitenga kwa siku 14, leo watarejea bungeni kuendelea na shughuli za kuwawakilisha wananchi, huku wakiendelea kuzingatia tahadhari zote za kujikinga na kuwakinga wengine,” amesema Mnyika.
Hata hivyo, wabunge hao wana kisiki cha kuruka mbele yao kwani Spika wa Bunge, Job Ndugai amewapa masharti ya kuwasilisha vipimo vya corona na kurejesha posho walizochukua kabla ya kuondoka bungeni ili wakidhi vigezo vya kurejea tena ndani ya nyumba hiyo ya wawakilishi.
Tangu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe atangaze Mei 1, 2020 kuwa wabunge wa chama hicho hawataingia bungeni kwa lengo la kuchukua hatua ya kujikinga na corona, kumekuwa na fukuto ndani ya chama hicho baada ya baadhi ya wabunge kukaidi agizo hilo.
Wabunge waliokaidi wamekumbwa na adhabu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa uanachama na wengine wakitakiwa kujieleza.
Wabunge hao ni Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini), Anthony Komu (Moshi Vijijini), David Kasilinde (Momba) na Joseph Selasini (Rombo).
Wabunge hao wamewasilisha barua kwenye Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kulalamika dhidi ya uamuzi wa chama hicho.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amekiri kupokea barua za wabunge hao na kwamba wanaendelea kuzifanyia kazi.
Watanzania watakiwa kujifunza kuishi na Corona
Mahakama ya Rufani yawaachia huru waliofungwa miaka 20 kwa ujangili