Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema kuwa hawatasusia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu, na kuwataka viongozi wanachadema na wananchi wote kuhamasishana kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura.
Amesema kuwa wananajua kuna baadhi ya watu wanatamani chama chao kisusie kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, lakini wanaamini kuwa wakisusia uchaguzi ni sawa na kususia maisha yao.
“ Tunatoa rai kwa watanzania, tusisusie uchaguzi huu, wenzetu wa upande wa pili wanatamani tususie. Kwa hizi siku 3 zilizoongezwa, viongozi wetu wa ngazi zote wahamasishane watoke kwa maelfu wakajiandikishe, tukisusa tutakuwa tumesusia maisha yetu kwa miaka mitano.” Amesema Mbowe
Ameyasema hayo leo alipozungumza na waandishi wa Habari makao makuu ya Chadema, Jijini Dar es salaam ili kueleza msimamo wao katika kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwakahuu.
Aidha ametoa ufafanuzi juu ya faida za kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na wananchi kushiriki.
“ Uchaguzi wa Serikali za mitaa unatupatia watu wanaosimamia maisha ya kila siku ya wananchi, mifumo ya huduma za kijamii na ndiyo ikulu ya wananchi. Ukizuia siasa matokeo yake utapata viongozi ambao hawana uhalali wa kuwaongoza wananchi kwa miaka mitano ijayo” amesisitiza Mwenyekiti huyo