Kiungo wa Simba SC, Clatous Chama amesema huu ni msimu wao wa kurudisha heshima na kubeba mataji yote ambayo wameyapoteza katika misimu miwili iliyopita.
Simba ni miongoni mwa timu zilizotumia gharama kuimarisha kikosi chake kufuatia mwenendo mbaya katika kipindi cha misimu miwili iliyopita ambayo hawakufanikiwa kubeba taji lolote na kushuhudia yakitua kwa mahasimu wao, Young Africans ukiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
“Msimu huu kuanzia uongozi pamoja na wachezaji, lengo letu ni kurudisha heshimna ya timu na mataji yote ya ndani ambayo tumeyapoteza kwenye misimu miwili iliyopita na hilo linawezekana kutokana na mikakati tuliyoiweka,” amesema Chama.
Amesema wana kikosi kipana chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa hivyo hata kama itatokea baadhi ya wachezaji wakakosekana kutokana na majeraha na masuala ya adhabu anaamini wachezaji wengine wana uwezo wa kuipa timu hiyo matokeo chanya.
Chama atakuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kitakachoivaa Young Africans katika Fainali ya Ngao ya Jamii kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kukosekana kwenye Nusu Fainali waliyocheza na Singida Fountain Gate kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyokuwa nayo.