Saa kadhaa zikisalia kabla ya kuikabili Jwaneng Galaxy katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kiungo kutoka nchini Zambia na klabu ya Simba SC Clatous Chama, amechimba mkwara mzito kuwa matokeo ya mchezo wa kwanza yamewapa ari ya kupambana zaidi.
Simba SC kesho Jumamosi (Desemba 02) inatarajia kuvaana na Janweng Galaxy katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa nchini Botswana saa kumi jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Simba SC inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupata matokeo ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya ASEC Mimosas uliopigwa Jumamosi iliyopita jijini Dar es salaam.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Chama amesema: “Kama wachezaji hatukutarajia matokeo ambayo tumeyapata katika mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Asec Mimosas.
“Lakini kama kikosi, matokeo haya yametufanya tuwe na ari zaidi ya kuhakikisha tunapambana kuelekea mchezo wetu wa pili dhidi ya Jwaneng Galaxy.
“Msimu uliopita tulianza kwa kusuasua, lakini tukafanikiwa kucheza Robo Fainali na sasa mwanzo mbaya wa msimu huu haimaanishi kuwa tumepoteza kila kitu bali tutahakikisha tunafikia malengo yetu.”