Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kuwa maafisa wa afya wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanatarajia kutambulisha chanjo ya pili ya ugonjwa wa Ebola mwezi ujao.
Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa na WHO, Serikali ya Kongo imetangaza mipango ya kuitambulisha chanjo ya pili ya majaribio iliyotengenezwa na kampuni ya Johnson na Johnson kuanzia katikati ya mwezi Oktoba.
Mkurugenzi wa kanda wa WHO, Matshidiso Moeti, amesema kuwa chanjo hiyo itasaidia kuhakikisha kwamba wana zana za kutosha kuzuia kuongezeka kwa mlipuko wa Ebola na pia nyenzo zinazofaa kuwalinda watu kabla ya ugonjwa kuzuka katika maeneo yaliyo hatarini.
Tangazo hilo limetolewa wakati ambapo madaktari wasio na mipaka wakiwa wanaishutumu WHO kwa kugawa chanjo ya kwanza ya Ebola nchini Kongo ambapo ziaidi ya watu 2,100 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.