Mazungumzo ya mkataba mpya baina ya Mshambuliaji Victor Osimhen na SSC Napoli yameripotiwa kusuasua na inadaiwa kuchangiwa na timu za Liverpool na Chelsea kumuhitaji staa huyo wa kimataifa wa Nigeria.

Osimhen ameanza msimu huu wa 2023-24 kwa kasi kubwa, akifunga mabao sita katika mechi nane za Serie A alizocheza hadi sasa, lakini amekuwa na shida nyingi za nje ya uwanja na klabu yake ya SSC Napoli.

Mwezi uliopita, kambi ya Osimhen ilitishia kuiburuza mahakamani SSC Napoli kutokana na kuposti video mbili za unyanyasaji kwa mshambuliaji huyo kwenye TikTok, ikiwamo moja ya kumdhihaki kwa kukosa Penati dhidi ya Bologna wakati nyingine ilikuwa kumfananisha na nazi.

SSC Napoli ilidai haikulenga kumuumiza Osimhen, huku jambo hilo likichochewa moto zaidi na uamuzi wa kocha Rudi Garcia kumtoa katika mechi dhidi ya Bologna.

Mapema mwezi huu, rais wa SSC Napoli, Aurelio de Laurentis alisema makubaliano ya awali ya mkataba mpya yalifikiwa kabla ya Osimhen kubadili mawazo ya kumwaga wino.

Kutokana na hilo, De Laurentiis alisema anafikiria kumpiga bei Osimhen mwakani kabla ya kufikia mwaka wa mwisho wa mkataba wake baada ya kuona pande hizo mbili kutokuwa na uhusiano mzuri.

Osimhen inaaminika analipwa Pauni 3.9 milioni kwa mwaka na anataka mshahara upande mara mbili ufike Pauni 78 milioni, lakini De Laurentiis hayupo tayari.

Mkataba wa Osimhen una kipengele kinachohitaji ilipwe Pauni 174.3 milioni kwa timu itakayohitaji huduma yake. Alitua SSC Napoli kwa Pauni 65.4 milioni mwaka 2020.

Kocha Azam FC hajakata tamaa na Ubingwa
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 30, 2023