Mlinda Lango Andre Onana amemtetea mchezaji mwenzake wa Manchester United Alejandro Garnacho baada ya Chama cha Soka cha England ‘FA’, kuanzisha uchunguzi kuhusu chapisho la mtandao wa kijamii lililotolewa na raia huyo wa Argentina akiwa na sokwe wawili juu ya picha ya kipa huyo wa Cameroon.

Garnacho aliandika chapisho hilo kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, baada ya Onana kuokoa Penati ya dakika za lala salama na kuipa United ushindi wa bao 1-0 dhidi ya FC Copenhagen kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mapema juma hili.

Muda mfupi baadaye ilifutwa baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 kufahamishwa na klabu kuhusu uwezekano wa kuhusishwa na ubaguzi wa rangi.

FA inachunguza tukio hilo na imemuita Garnacho kwa uchunguzi wake.

Alejandro Garnacho ameichezea Manchester United mechi 11 hadi sasa msimu huu.

Juzi Alhamisi (Oktoba 26), Onana alimtetea Garnacho katika chapisho lake kwenye mtandao wa kijamii.

“Watu hawawezi kuchagua kile ninachopaswa kuchukizwa nacho,” aliandika Onana kwenye Instagram.

“Ninajua hasa Garnacho alichokuwa anamaanisha, Jambo hili halipaswi kwenda mbali zaidi.”

Endapo itabainika alikusudia Ubaguzi wa Rangi, Garnacho anaweza kufungiwa kwa kukiuka sheria za Chama cha Soka nchini England ‘FA’.

Mnamo 2019, kiungo wa kati wa Manchester City, Bernardo Silva alifungiwa mechi moja na kutozwa faini ya Pauni 50,000 na FA baada ya kumlinganisha Benjamin Mendy na katuni nyeusi, licha ya tume kukubali hakukusudia kuwa mbaguzi wa rangi.

Mwaka 2021, mshambuliaji wa United, Edinson Cavani alipewa adhabu ya kutocheza mechi tatu na kutozwa faini ya Pauni 100,000 kwa chapisho la mtandao wa kijamii ambalo lilikuwa na neno la Kihispania ambalo lingeweza kutafsiriwa kama ubaguzi wa rangi nchini England.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Oktoba 29, 2023
Victor Osimhen: Bora Marekani kuliko Saudia