Aliyekua Meneja wa Klabu bingwa nchini Italia Inter Milan, Antonio Conte, amealiangushia lawama benchi la ufundi la Chelsea linaloongozwa na Thomas Tuchel, kwa kusema limeshindwa kumtumia Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji Romelu Lukaku.
Conte amesema kwa muda mrefu amefanya kazi na Mshambuliaji huyo, na alionesha uwezo mkubwa kisoka na kufunga mabao, tofauti na sasa ambapo amekua hafungi kwa kasi aliyoizoea.
Amesema kuna haja kwa benchi la ufundi la klabu hiyo ya jijini London ambayo amewahi kuitumikia, kujitafakari kwa kina na kujua namna ya kumtumia Lukaku, ambaye amedai ana kila sababu ya kuisaidia Chelsea msimu huu.
“Nadhani ana uwezo wa kufanya vizuri zaidi, ukiacha vyote mbinu zake. Yupo katika ubora mkubwa sana, lakini mchezaji anapaswa kuboresha kiwango chake mpaka pale atakapostaafu,” amesema Conte aliiambia Sky Sport Italia.
“Wakati wa mchezo, kuna muda Lukaku anapaswa kurudishwa mchezoni, lakini zaidi ya hivyo ni mmoja kati ya mshambuliaji hatari kucheza dhidi yake, kwa sababu anaweza kufanya hatari eneo lolote katika uwanja.
“Ukiwa na mshambuliaji kama yule, unahitaji kumtumia na sidhani kama Chelsea wameweza kutambua njia ya kumtumia mpaka sasa.” ameongeza Conte.
Romelo Lukaku alisajiliwa kwa mara ya pili huko Stamford Bridge wakati wa majira ya kiangazi kwa kitita cha Pauni milioni 98, baada ya kuonesha uwezo wa ajabu akiwa na Inter Milan ya Italia.