Klabu ya Chelsea inataka kufanya utekaji kwa mchezaji nyota wa Paris Saint Germain (PSG), Kylian Mbappe, kuipiku Liverpool.

Chelsea inafuatilia nyendo za Mbappe, ambaye ameweka ngumu kutia saini mkataba mpya PSG, akiishinikiza klabu hiyo ya Ligi Kuu Ufaransa kuondoka.

Awali, Mbappe alikuwa na mpango wa kutua kwa matajiri wa Santiago Bernabeu Real Madrid ya Hispania, lakini mpango huo unasuasua baada ya idadi ya klabu za Ulaya kumtupia ndoano.

Kocha wa Chelsea Mauricio Pochettino, amejitosa kuwania saini ya Mbappe, ambaye Mkataba wake unamalizika Juni, mwakani.

Wakati Muargentina huyo akimvutia kasi Mbappe, Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, alitangulia kuweka bayana dhamira ya kutaka huduma ya nyota huyo.

Pochettino Anataka kuisuka upya Chelsea yenye maskani yeke Stamford Bridge, baada ya msimu uliopita kumaliza ligi kwa aibu ikiwa nafasi ya 12.

Thamani ya Mbappe imetajwa ni Pauni Milioni 200, hivyo Chelsea au klabu inayomtaka inatakiwa kuvunja benki kupata saini yake.

Mbappe amekuwa na mvuto mkubwa, baada ya kufunga mabao 191 mechi zaidi ya 200 alizocheza za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Taarifa za Mbappe zimekuja wakati mpachika mabao huyo akikataa ofa nono ya pauni milioni 259 iliyowekwa mezani na matajiri wa Saudi Arabia klabu ya Al-Hilal.

Hata hivyo, Mbappe amekataa kujiunga na klabu hiyo pamoja na kuahidiwa kitita hicho ambacho kingemfanya kuwa mchezaji ghali duniani.

Itakumbukwa kwamba Mbappe mwenye miaka 24, aliwahi kuonyesha mapenzi yake Liverpool mwaka 2018, baada ya kutamka anaipenda klabu hiyo ya Anfield.

Mshambuliaji huyo alisema sababu ya kuipenda Liverpool, ni kutokana na mama yake kuwa mpenzi mkubwa wa klabu hiyo.

“Tulizungumza kwa kifupi, lakini haikuwa sana, alisema Mbappe alipohojiwa na gazeti la Telegraph mwaka jana.

“Niliitaja Liverpool kwa sababu mama yangu anaipenda Liverpool”. Mchezaji huyo alisema

Liverpool ni klabu kubwa na amewahi kukutana nayo mara tano katika mechi mbalimbali tangu akiwa AS Monaco kabla ya kujiunga PSG.

Mtaji UTT AMIS wafikia Trilioni 1.5
Mayele: Sijaondoka Young Africans kwa ubaya