Eva Godwin – Dodoma.
Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoa wa Dodoma imeshauriwa kufuatilia kwa umakini vyanzo vyote vilivyopo katika Wilaya hiyo, ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Hayo yamebainishwa hii leo Oktoba 23, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutathmini, kukagua na kufanya ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo kwa Kipindi cha Julai hadi Septemba 2023.
Amesema, “niwapongeze kwa kufanya vizuri kwenye kusimia miradi na ongezeko la mapato Katika Wilaya ya Chemba ni vizuri kwenda kwa kasi hiyo na kila mtu afanye kwa ngazi ya Idara ili kuleta mabadiiliko zaidi kwa kila sekta.”
“Kila baada ya Miezi mitatu kutakuwa na mambo ya ufuatiliaji wa mapato ili kuona Kwanini miradi mingine imekuwa changamoto kwa mapato ya Halmashauri,” amesema Senyamule.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Prosister Tairo amesema katika mwaka wa Fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Chemba imepanga kukusanya na kutumia kiasi cha fedha cha Shilingi Bilioni 28.7.
“Na katika kipindi cha robo ya kwanza Julai hadi Septemba Halmashauri ilipanga kukusanya Shilingi Bilioni 7.1 kutoka katika vyanzo vyote vya mapato Wilayani,” amesema Tairo.
Ameongeza kuwa, “na hadi kufikia Septemba 2023 Halmashauri imekusanya Bilioni 7.4 sawa na asilimia 103 ambapo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba Jumla ya Shilingi Bilioni 5.3 zimetumika.”