Watu watano wamekufa na makumi wamejeruhiwa baada ya jengo la ghorofa la kibiashara jijini Shanghai nchini China kuanguka wakati wa matengenezo, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya nchi hiyo.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa tano na nusu katikati ya jiji hilo ambapo watu kitengo cha uokoaji kimeeleza kuwa watu 20 wameripotiwa kunasa kwenye vifusi.
Hata hivyo, vyanzo vingine vimeeleza kuwa na idadi tofauti ya vifo lakini serikali ya jiji hilo pamoja na wizara ya dharura kwa pamoja wamekaririwa wakitaja idadi ya vifo vya watu watano.
Ingawa vyombo husika havikueleza kiundani kuhusu hali ya majeruhi na idadi yao, picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonesha damu pamoja na anguko kubwa la vifusi.
Jeshi la polisi lilizingira eneo hilo na kuweka ulinzi mkali kuhakikisha hakuna picha za ziada zitakazochukuliwa bila kuwa na kibali maalum.
Kwa mujibu wa kitengo cha uokoaji, jengo hilo lilikuwa linatumiwa na kiongozi wa magari ya Mercedes-Benz.
Mmoja kati ya wakaazi wa eneo hilo ameiambia AFP kuwa alikuwa amelala kisha akasikia mtetemo kama wa tetemeko la ardhi, kisha akasikia kishindo kikubwa.
“Nilidhani ni mlipuko wa bomu mara ya kwanza,” alisema mwanamke mmoja ambaye ni mkazi wa eneo hilo. Picha za juu zinazoonesha tukio hilo zinaonesha karibu nusu ya paa la jengo hilo ilianguka.