Katika hali ya kushangaza Mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Ranga Chivaviro amepiga chini ofay a Randi milioni 3 za Afrika Kusini ambazo ni sawa na shilingi 358,737,000 za Tanzania ili asajiliwe na Klabu ya Al-Akhdar ya nchini Libya.
Chivaviro anatajwa huenda akasajiliwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, baada ya kufikia makubaliano na mabosi wa timu hiyo, ambaye atakuja kuwa mbadala wa Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Mayele anayetajwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Chivaviro pia alikuwa ananyemelewa na miamba ya soka Afrika Kusini Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo nayo ilipeleka ofa nono ya kumtaka, lakini akaichomolea.
Mtandao mmoja wa michezo kutoka Afrika Kusini, umeripoti kuwa Al-Akhdar wameonesha nia kubwa ya kumsajili mshambuliaji huyo aliyekuwa anachuana na Mayele katika ufungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu 2022/23.
Mtandao huo umefafanua kuwa mshambuliaji huyo amegomea kitita hicho cha fedha alichotengewa kutokana na yeye mwenyewe kuonesha nia kubwa ya kutua Young Africans.
Nyota huyo atajiunga na Young Africans kama mchezaji huru, mara baada ya mkataba wake kumalizika wa kuichezea Marumo Gallants ambayo imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Rais wa Young Africans Injinia Hersi Said, hivi karibuni alizungumzia ishu ya usajili kwa kusema: “Tunakaribia kumalizana na mmoja wa washambuliaji wakubwa wa nchini Afrika Kusini ambaye jina lake ni siri kwa sasa.”