Baadhi ya Wachezaji wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans bado wana matumaini ya kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, licha ya kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali wa Michuano hiyo.
Young Africans juzi Jumapili (Mei 28) ilikubali kufungwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam mabao 2-1, dhidi ya USM Alger, ambao watakuwa nyumbani nchini Algeria katika mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa Jumamosi (Juni 03).
Wachezaji walionesha kuwa na matumaini ya kwenda kupata ushindi ugenini na kurejea Tanzania na Ubingwa wa Afrika ni Washambuliaji Fiston Mayele na Kennedy Musonda, ambapo kwa nyakati tofauti wamesema bado timu yao ina nafasi ya kushinda mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika watakapocheza nchini Algeria dhidi ya USM Alger.
Young Africans wanahitaji ushindi wa uwiano wa mabao 2-0 ili wajihakikishie kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Mshambuliaji Kennedy Musonda, amesema kuwa wana dakika nyingine 90 za ugenini za kuipambania Young Africans na kuandika rekodi ya kubeba kombe hilo.
Musonda amesema kuwa kama wachezaji wameumizwa na matokeo hayo waliyoyapata nyumbani, ambayo yatawafanya waongezee bidii ya kuipambania timu na kupata matokeo ya ushindi.
“Tunafahamu mashabiki wa Young Africans wameumizwa na matokeo ya kufungwa nyumbani, pia sisi tumeumia, hivyo wasikate tamaa, tuwaombe waendelee kutusapoti tutakapokwenda kurudana ugenini,” amesema Musonda
Neye Kinara wa mabao katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu, Fiston Mayele ambaye amepachika mabao saba, amesema kuwa mara baada ya mchezo huo walikwenda kufanya kikao, kikubwa ni kukumbushana kwenda kulipa kisasi Algeria.
“Mashabiki wetu wasikate tamaa kwa kupoteza mchezo wa kwanza wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwani bado tunayo nafasi ya kushinda mchezo wa marudiano.
“Haitakuwa kazi nyepesi kwetu, lakini kwa nguvu za Mungu, ninaamini tunakwenda kupata matokeo mazuri ya ushindi ugenini. Kwani kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo huo,” amesema Mayele