Kampuni ya Uwakala ya TNB Sports Agency Management inayomsimamia Mshambuliaji wa Marumo Gallants ya Afrika Kusini Ranga Chivaviro, imethibitisha kupokea ofa kutoka kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans na Azam FC.
Chivaviro, anatajwa kuwania na klabu hizo za jijini Dar es salaam, baada ya kuonesha kiwango kikubwa katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku timu yake ya Marumo Gallants ikitolewa hatua ya Nusu Fainali kwa kufungwa na Young Africans jumla ya mabao 4-1.
Mkurugenzi wa TNB Sports Agency Management Herve Tra Bi, amethibitisha kupokea ofa kutoka Young Africans na Azam FC, lakini amesisitiza huenda Mshambuliaji Ranga akatua kwa wananchi kutokana na ofa yao kuwa nzuri zaidi.
Amesema wakati wowote Rais wa Young Africans Injinia Hersi Said anatarajiwa kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kuanza mazungumzo na Uongozi wa Kampuni hiyo pamoja na Uongozi wa Marumo Gallants ambayo mwishoni mwa juma lililopita iliporomoka daraja huko Afrika Kusini.
“Ni kweli tunaendelea na mazungumzo na Young Africans juu ya Uhamisho wa Ranga Chivaviro, mchezaji aliyefanya Vizuri kwenye michuano ya CAF ni wazi hawezi kukubali kubakia ikiwa timu imeshuka daraja, tunaipa kipaumbele timu inayocheza michuano ya CAF, tumepokea Ofa kutoka Young Africans na Azam FC na bado hutujafikia makubaliano”
“Ofa Young Africans ni Nzuri na Rais Hersi Saidi ametupa Ofa nzuri na ni furaha kwa Ranga kuja Tanzania, kiongozi wao atakuja hapa siku chache kumalizia makubaliano natumai na sisi tutakuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya mambo endapomambo yatakuwa sawa katika mazungumzo yetu ya mwisho.” amesema Herve Tra Bi
Young Africans inatajwa kujiandaa kumsajili Mshambuliaji kuelekea mwishoni mwa msimu huu, huku taarifa zikieleza huenda Fiston Kalala Mayele akauzwa kwenda katika moja ya klabu ambazo zimeonesha nia ya kutaka kumsajili.
Mayele anatajwa kuwa katika rada za Klabu za Orlando Pirates (Afrika Kusini), RS Berkane na Raja Casablanca (Morocco) baada ta kuonesha kiwango maridhwa kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23, huku akiifungia Young Africans mabao sita hadi sasa.
Mshambuliaji mwingine aliyefunga mabao mengi katika Michuano hiyo ni Ranga Chivaviro, ambaye anatajwa kuwaniwa na Young Africans, ambayo haitaki kufanya kosa la kuziba nafasi ya Meyele endapo ataondoka mwishoni mwa msimu huu.