Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo ameelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, kwa vitendo, kuboresha huduma za uchukuzi, usafiri na usafirishaji katika Ziwa Tanganyika, ambapo kufikia mwezi Desemba, 2023, Wananchi wataanza kupata nafuu, kuelekea kumalizika kwa adha kubwa iliyopo sasa.

Chongolo ametangaza mikakati hiyo, alipokuwa akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kalambo, Jumatatu Oktoba 9, 2023, ambapo anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Rukwa, yenye malengo ya kuhamasisha uhai wa CCM, kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, kwa kutembelea miradi ya maendeleo.

Amesema, unafuu huo utatokana na kukamilika kwa matengenezo ya moja ya meli, kati ya mbili zilizopo sasa, Mv Mwongozo na Mv Liemba, ambazo zote zinafanyiwa matengenezo, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu na kutengeneza meli mpya kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na Wananchi itakayoondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika.

“Wote ni mashahidi hizi meli (Mv Liemba na Mv Mwongozo), zimetengenezwa miaka mingi, ingawa Mwongozo sio ya miaka mingi sana kama Liemba. Juzi nikiwa Katavi nimezungumza na Waziri wa Uchukuzi, tumekubaliana mambo kadhaa ikiwa ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” amesema Chongolo.

Aidha, amesema Serikali imejenga bandari za mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambapo kuna Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kasanga zilizoko mkoani Rukwa, Bandari ya Karema ambayo iko Katavi, pamoja na Bandari ya Kigoma, huku akibainisha kuwa hata bandari zingine ndogo ndogo zinawekewa mipango ili zifanye kazi ya kurahisisha shughuli za usafiri, usafirishaji na uchukuzi.

Katika ziara yake Wilayani Kalambo, Chongolo alishiriki Mkutano wa Shina Namba sita Singiwe, kutembelea na kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, kutembelea na kukagua Bandari ya Kasanga, kukagua ujenzi wa Barabara ya Matai – Kasesya na kuzungumza na Wananchi katika maeneo yote ikiwemo na Kisumba.

Athari za Mvua: Maporomoko ya ardhi yauwa 23
Miradi uhifadhi, usimamizi Mazingira kuibuliwa katika jamii