Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Ndugu Daniel Chongolo amesisitiza kauli ya chama hicho kuitaka Serikali kuongeza kasi ya suala la uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari ili hatua za uwekezaji ziende katika hatua nyingine na Watanzania wote waanze kuona matokeo chanya kupitia mikataba ya utekelezaji.
Amesema kuwa suala la uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam, ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, akiwataka Wanachama na Viongozi wa CCM kuwa makini na wapinzani wa mradi huo wanaopita kupotosha wananchi, kwa sababu wanahofia iwapo CCM ikitekeleza kwa ufanisi kila ilichoahidi kwa wananchi kupitia ilani hiyo yenye kurasa 303, watakosa agenda.
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesema hayo leo Jumapili Julai 16, 2023, alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara Mjini, ukiwa mwendelezo wa ziara yake, ambayo ameitumia kufafanua masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali kupitia Ilani ya CCM yam waka 2020 – 2025, ikiwemo suala la makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai yanayolenga kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uboreshaji wa uendeshaji wa Bandari ya Dar Es Salaam.
Kauli hiyo ya Ndugu Chongolo imekuja siku moja, baada ya kuitoa awali wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano mwingine mkubwa uliofanyika siku ya Jumamosi, Julai 15, 2023 katika Uwanja wa Rwandanzovwe, Mbeya Mjini, ambapo alisema CCM kinaitaka Serikali kuharakisha suala hilo liende hatua za utekelezaji utakaoanza kutoa matokeo chanya na kuweka bayana kuwa kazi ya kujibishana na wanasiasa wanapotosha wananchi, itafanywa na Chama hicho kwa sababu ndicho kiliomba na kikapewa dhamana ya kushika dola, kuunda Serikali na kuongoza nchi, kupitia sanduku la kura mwaka 2020.
Akizungumzia leo mbele ya maelfu ya wananchi waliofika katika mkutano huo uliofanyika Mtwara Mjini, Ndugu Chongolo amesema kinachofanyika ni utekelezaji kwa vitendo wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na sio vinginevyo, huku akiwataka wanachama wa CCM kuwa makini na watu wanaokwepa kujadili utekelezaji wa ilani hiyo badala yake wanazusha maneno na kufanya siasa za kutaka kuwachonganisha na viongozi wao.
“Rais (Dkt. Samia Suluhu Hassan) kwa dhamana ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, anaongoza njia…anaongoza wanaCCM, lakini yote ni makubaliano na maagizo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na si vinginevyo. Wapo watu wanahangaika, wanatumia nguvu kubwa sana, kuhamisha masuala ya msingi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwenda kwa mtu.”
“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, yenye kurasa 303, ndiyo iliyoahidi barabara kutoka Masasi kuja Newala mpaka kufika hapa Mtwara Mjini, mbona tukienda kujenga hawahoji kwanini mnasaini mjenge hiyo barabara? Kwanini wanahoji mambo machache, mengine wanayaacha? Kwa sababu wanajua wakiacha tukatekeleza yote kwa ufanisi, kazi yao ni ngumu huko mbele, ndiyo maana wanahangaika kuchonganisha,” amesema Katibu Mkuu Ndugu Chongolo.
“Sasa niwaambie…ukichukua Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ukiangalia ibara ya 22 inaeleza namna mipango ya uwekezaji ikiwemo kwenye bandari ilivyoandikwa na kuainishwa wazi. Lakini ukienda kwenye ibara ya 59, ukurasa wa 92 wa Ilani yetu imeweka wazi kwa kuainisha namna mipango ya uwekezaji ilivyo kwenye banadari nchini.”
Ndugu Chongolo ambaye katika ziara hiyo ameongozana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndugu Steven Wassira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo na Mbunge wa Jimbo la Ukonga (CCM), Ndugu Jerry Silaa wakitoa ufafanuzi wa kina kuhus ukweli na uhalisia wa mjadala wa mkataba wa uboreshaji utendaji wa bandari na manufaa yake.
Ameongeza kuwa wapo watu wanahangaika kuhamisha agenda, ikiwa ni mbinu ya kuwafanya baadhi ya Wanachama CCM wasione kuwa kinachoenda kutekelezwa katika suala la uwekezaji wa kuboresha utendaji wa bandari ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambacho ndicho chama kilichopewa dhamana ya kuongoza nchi na uwekezaji huo hatimae utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania na nchi nzima kwa ujumla.
“Hawataki mjadili ilani, na kwamba hili ni utekelezaji wa ilani, ili ninyi mbakie mkifikiria linalotekelezwa sio la kwenu. Hili linalotekelezwa ni la CCM. Ni ahadi ya CCM na tunatekeleza wanaCCM kwa sababu ndiyo tuliopewa dhamana ya kuongoza nchi. Hatuna msalia mtume, hatuna hofu, hili jambo tutalitekeleza kwa sababu ni utekelezaji wa ilani yetu ya uchaguzi,”
“Wanaohangaika kulihamisha na kulifanya liwe la Mheshimiwa Rais, liwe la Mwenyekiti, wamekosea muda, wamekosea move, wamekosea mwelekeo wa kulifanya liende huko wanakotaka. Tumewagundua, tunawajua, tunajua njia wanazotumia. Na ndiyo maana tunaitwa Chama tawala nchini. Mnaona kuna mtu amekaa kienyeji? Kuna mtu ana mashaka? Wajifunze kwamba kuongoza nchi si kazi ya lelemama. Kupepeta mdomo ni kazi rahisi. Kutenda ni kazi yenye wajibu,” amesema Ndugu Chongolo.
“Hapa ninyi ni mashahidi. Hebu ukiwa unaangalia mpira. Kila mmoja huwa anakuwa mjuzi. Anawaambia pale angefanya hivi…angegusa kidogo…nenda uwanjani kajaribu. Tuone utakavyogusa na kuingiza hilo goli. Kazi sio rahisi…mdomo nje…ushabiki, uzushi, uchonganishi ni kazi rahisi. Lakini kazi ya kutenda ni kazi ngumu. Haina lelemama. Haitaki tukae kienyeji.”
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amesisitiza kuwa CCM iko imara na timamu katika kusimamia utekelezaji wa masuala yote kiliyoahidi kwa wananchi, huku akiwataka Wanachama na Viongozi wa CCM kuisoma ilani kwa makini na kuwaelimisha wengine ili waache kukubaliana na mambo rahisi yanayotengenezwa ili kuwachonganisha.
“Uwanja wa ndege wa hapa mambo mazuri, ule wa Ruvuma mambo mazuri, bado pale Lindi, niwahakikishie mambo yakitunyookea, mapato yakiongezeka, tunashindwaje kuongeza hata wa Newala ukawa uwanja mkubwa wa kisasa. Suala ni uwezo. Kwa hiyo Niwahakikishie na nisisitize. Tuko imara. Tuko timamu.”
“Wala hatuna haja ya kutumia muda mwingi. Najua wanaCCM mnajitambua. Mnajua dhamana yenu, najua mna dhamana na wajibu wa kuisimamia Serikali itekeleze ilani inavyotakiwa. Turudi tusome, tuelimishe wenzetu. Tusimamie hapo hapo. Tuache kukubaliana na mambo rahisi ya kuchonganishwa na kuchonganishwa na viongozi wetu. Lazima tuwalinde, lazima tusimamie na tuhakikishe mambo yanatokea.”