Kiungo wa Dodoma Jiji FC, Christian Zigah ameongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Dodoma Jiji msimu ujao.
Mchezaji huyo alisajiliwa akitokea Biashara United pamoja na Collins Opare na Hassan Mwaterema.
Licha ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia msimu uliopita bado ameendelea kuwa chaguo namba moja katika nafasi ya kiungo kwa kocha Melis Medo.
Kiungo huyo alikuwa akicheza na Salmin Hoza, Rajabu Mgalula na Enrick Nkosi katika nafasi ya kiungo.
Akizungumza baada ya kukamilisha mpango wa kusaini mkataba mpya Zigah amesema anashukuru mungu kwa kufanikisha mpango huo na ana matarajio makubwa ya kuisaidia Dodoma Jiji Fc msimu ujao 2023/24.
“Nimeshamalizana na Dodoma Jiji,” alisema kwa kifupi kiungo huyo ambaye anasifika kwa uwezo wake wa kuchezesha timu na inadaiwa baadhi ya timu zilikuwa zikihitaji huduma yake.
Mmoja ya viongozi wa Dodoma ambaye hakutaka kutajwa jina lake amesema Zigah tayari amesaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
“Ukitaka ukosane na Medo kama angeondoka Zigah yule ni chaguo lake namba moja anampenda na anauelewa uwezo wake,” amesema kiongozi huyo.