Kiungo wa Zamani wa klabu za Coastal union, Young Africans na Simba SC Athumani Iddi “Chuji” amewatupia lawama wadau wa soka mkoani Singida, kwa kusema wamekua chachu ya timu yao ya Singida United kukosa matokeo mazuri msimu huu wa 2019/20.
Singida United ipo kwenye hatari ya kushuka daraja kutokana na muendelezo wa matokeo mabovu, yaliyoiandama klabu hiyo iliyopanda na kucheza ligi kuu misimu miwili iliyopita.
Mpaka ligi kuu inasimamishwa kupisha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya Corona Singida United inaendelea kushika mkia katika msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha alama 15, huku ikibakisha michezo tisa.
Chuji amesema wadau wa soka mkoani Singida hawana uzalendo wa kweli na mara kadhaa wameonyesha kutokua pamoja na viongozi wa serikali na klabu, ambao wanaendelea kupambana ili kuhakikisha timu haishuki daraja.
“Nashangaa watu wa Singida siyo kama wa Mtwara ambako Ndanda FC kila mwaka inapokuwa kwenye hali mbaya, basi wanakwenda kwa viongozi wa mkoa kama vile Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa kisiasa kuhamasisha wananchi timu kuwa haishuki na wanafanikiwa sana kwa hilo, Ndanda huwa inasalimika kwa kubakia Ligi Kuu, nashangaa kwa nini watu Singida hawafanyi hivyo.” Amesema Chuji
Wakati huo huo Chuji aliyesajiliwa na Singida United wakati wa dirisha dogo la usajili mwishoni mwa mwaka jana, amethibitisha kuvunja mkataba na klabu hiyo kwa sababu ya kutolipwa mshahara wa miezi mitatu.
“Kwa sasa niko huru kwa sababu nilisajiliwa kumalizia ligi kipindi cha dirisha dogo, lakini hadi naondoka nilikuwa sijalipwa miezi mitatu”, alisema chuji.
Licha ya kuvunja mkataba lakini anashangazwa na watu wa Singida ambao hawajaonyesha ishara yoyote baada ya timu hiyo kuonekana kuwa katika hali hatarishi ya kushuka daraja.