Kabla ya kuwakabili Mtibwa Sugar leo jioni, Kocha Mkuu wa Azam FC Aristica Cioaba, ametamba kupitia rekodi yake ya kushinda micheza saba mfululizo ya Ligi Kuu msimu huu 2020/21.
Azam FC leo Jumatatu Oktoba 26 watacheza mchezo wa mzunguuko wa nane wa Ligi Kuu kwenye uwanja wa ugenini mjini Morogoro, huku dhamira yao ikiwa ni kushinda mchezo wa nane mfululizo.
Kocha Cioaba, amesema wataingia kwenye mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro, wakiwa na rekodi nzuri ya kushinda michezo saba iliyopita, hivyo anaamini morari ya wachezaji wake ipo juu, na wanahitaji kuendelea kuwa kwenye furaha ya ushindi.
“Tunaingia tukiwa tumeshashinda mechi saba, tuendeleze umakini ili tusije kuupoteza mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar, mpango wetu ni kujitahidi kuchukua alama zote kwenye kila mchezo.” Amesema Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba
Azam FC itawakosa nyota wake wawili ambao wamehusika kwenye mabao saba kati ya 14 ambayo yamefungwa na timu hiyo inayonolewa na kocha kutoka nchini Romania Aristica Cioaba.
Mshambuliaji Obrey Chirwa mwenye mabao manne na pasi mbili za mabao anasumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu huku kiungo Salum Abubakar, ‘Sure Boy’ mwenye pasi moja ya bao, akitumikia adhabu ya kuoneshwa kadi tatu za njano.
Azam FC imeshacheza michezo saba na kuvuna alama 21 zinazowaweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, huku Mtibwa Sugar ikicheza michezo saba na kuambulia alama nane zinazoiweka kwenye nafasi ya 15.
Michezo mingine ya Ligi Kuu inayochezwa leo Jumatatu Oktoba 26.