Vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC, leo Jumatatu Oktoba 26 watashuka dimbani kucheza mchezo wa mzunguuko wa nane wa ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar, ambao watakua nyumbani kwenye Uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro.

Azam FC waliwasili mjini humo jana Jumapili Oktoba 25 na kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mpambano huo, unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kufuatia hitaji la alama tatu muhimu kwa timu zote mbili.

Hata hivyo Azam FC itawakosa nyota wake wawili ambao wamehusika kwenye mabao saba kati ya 14 ambayo yamefungwa na timu hiyo inayonolewa na kocha kutoka nchini Romania Aristica Cioaba.

Mshambuliaji Obrey Chirwa mwenye mabao manne na pasi mbili za mabao anasumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu huku kiungo Salum Abubakar, ‘Sure Boy’ mwenye pasi moja ya bao, akitumikia adhabu ya kuoneshwa kadi tatu za njano.

Mkuu wa Idara Ya Habari Na Mawasilino Ya Azam FC, Zakaria Thabit (Zaka Zakazi) amesema wana imani kubwa kikosi chao kitafanya vyema dhidi ya Mtibwa Sugar licha ya kuwakosa nyota wawili kikosi cha kwanza.

“Tutawakosa wachezaji wawili ambao ni Chirwa (Obrey) na Sure Boy licha ya kwamba hawatakuwepo bado tumejipanga kupata ushindi kwenye mchezo wa leo,” amesema.

Azam FC imeshacheza michezo saba na kuvuna alama 21 zinazowaweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, huku Mtibwa Sugar ikicheza michezo saba na kuambulia alama nane zinazoiweka kwenye nafasi ya 15.

Masau Bwire: Simba SC watakutana na mpira KAUKAU
IGP Sirro atahadharisha vurugu Arusha