Kiungo kutoka nchini Italia Claudio Marchisio, ameachana na mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC, baada ya kuweka historia ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka 25.
Kiungo huyo mwenye umri wa kiaka 32, alianza kuitumikia klabu hiyo katika ngazi ya vijana mwaka 1993, akiwa na umri wa miaka saba, na kwa kipindi chote amekua kivutio kwa mashabiki wa Juventus FC.
“Tunashukuru kwa mchango wake mkubwa alioutoa klabuni hapa kwa muda mrefu, tutaendelea kuwa naye bega kwa bega katika maisha yake baada ya kuondoka hapa.” Imeeleza taarifa iliyotolewa na klabu ya Juventus.
Marchisio ambaye ni mzaliwa wa mjini Turin yalipo makao makuu ya klabu ya Juventus, amelazimika kuachana na klabu hiyo kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita.
Anaondoka Juventus akiacha kumbukumbu ya kuwa miongoni mwa wachezaji walipata mafanio makubwa kwa kutwaa mataji saba ya ligi kuu ya Italia (Serie A), mataji manne ya kombe la Italia (Coppa Italia), mataji mawili ya Supercoppa Italiana na taji la ligi daraja la kwanza (Serie B).
Mpaka hii leo anaamua kuondoka klabuni hapo, tayari ameshacheza michezo 389 na kufunga mabao 37.