Kwa mara nyingine tena Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limemteuwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Clifford Mario Ndimbo, kuwa Afisa Habari wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi kati ya Simba SC ya Tanzania dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Timu hizo zitakutana Jumamosi (Machi 18) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Simba SC ikitarajia kuutumia mchezo huo kama ngazi ya kuelekea Hatua ya Robo Fainali, endapo itapata ushindi wowote.
Shirikisho la Soka Tanzania limetoa taarifa za uteuzi huo katika vyanzo vya Habari vya Shirikisho hilo leo Jumatatu (Machi 13).
“Ofisa Habari na Mawasiliano TFF, @clifordmariondimbo ameteuliwa na CAF kuwa Ofisa Habari wa mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) Simba SC (Tanzania) vs Horoya AC (Guinea) utakaochezwa Machi 18, 2023 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. “ imeeleza taarifa hiyo
Ndimbo aliteuliwa kuwa Afisa Habari wa mchezo wa Mzunguuko wanne uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam juma lililopita kati ya Simba SC dhidi ya Vipers SC ya Uganda.
Mchezo huo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka na ushindi wa 1-0, ambao uliifanya timu hiyo kufikisha alama 06 katika msimamo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ikitanguliwa na Raja Casablanca ya Morocco iliyojizolea alama 12.
Horoya AC ya Guinea inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 04, huku Vipers Sc ya Uganda inabuza mkia wa Kundi hilo kwa kuwa na alama 01.