Wizara ya Afya nchini Kenya imesema kuwa kuanzia Jumatatu ijayo, Hospitali ya Nairobi itafanya vipimo vya corona ikiwa imewezeshwa kupima sampuli 900 kwa siku moja. Imeeleza kuwa gharama za upimaji ni Sh.10,000 za Kenya (Sawa na Shilingi 215,000) kwa kila sampuli.
Gharama hizo zinahusisha kulipia baadhi ya vifaa vya kupimia pamoja na vifaa vya kujilinda vya madaktari watakaofanya vipimo hivyo. Madaktari wanapaswa kuvalia mavazi yanayoweza kuwalinda dhidi ya mambukizi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya Kenya iliyokaririwa na Citizen, vipimo vitachukua kati ya saa 6 hadi 24 hadi kupata majibu. Watakaokutwa na virusi vya corona watapaswa kukaa karantini ndani ya hospitali hiyo kama wataona inafaa, na Wizara ya Afya itawafuatilia kwa ukaribu.
“Kwa sasa hospitali ina uwezo wa vitanda 37 vinavyoweza kutumiwa na watu walioathirika na virusi vya corona kwa kuwapa nafasi nzuri, vitanda 12 kwa ajili ya watakaokuwa ICU lakini tuna mpango wa kuongeza,” taarifa ya Wizara ya Afya inaeleza.
Imeongeza kuwa timu ya wataalam wa afya katika hospitali hiyo waliopewa mafunzo na wenye nidhamu ya kazi watahusika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Nairobi, Dkt. Allan Pamba amesema, “tunawakaribisha watu wote kuja na kufanya vipimo ili kupunguza maambukizi kwa jamii. Tunaomba ushirikiano wa wadau kuungana nasi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha upimaji wa watu wengi zaidi.”
Hadi Aprili 29, 2020, Kenya ilitangaza kuwa na visa vya corona 363.