Wakati Dunia inaendelea kutafuta dawa na kinga dhidi ya virusi vipya vya corona (covid-19), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu ya Tanzania, (NIMR) imetengeneza ‘tiba lishe’ ya asili ya kuwasaidia wagonjwa kwa kutibu dalili zinazotokana na ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Tiba Asili cha NIMR, Dkt. Justine Omolo amesema kuwa taasisi hiyo imetayarisha ‘mchanganyiko (formula)’ ya tiba lishe ambayo itasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona kwa kutibu dalili zinazotokana na ugonjwa huo, lakini wataifanyia majaribio ya kisayansi kabla ya kuanza kuitumia rasmi.
“Mchanganyiko wa tiba lishe hiyo sio dawa ya corona, lakini inasaidia kumpa nafuu mgonjwa wa corona kwa kutibu dalili zinazoambatana na ugonjwa huo,” Dkt. Omolo aliiambia Daily News.
Dkt. Omolo aliongeza kuwa tayari wameanza kufanya taratibu za kupata kibali cha kufanya majaribio ya tiba lishe hiyo.
Alisema kuwa kama tiba lishe hiyo itapata majibu chanya ya kisayansi watalijulisha Shirika la Afya Duniani (WHO) kwakuwa tayari itakuwa na uthibitisho wa kisayansi.
Jana, WHO ilitoa taarifa ambayo ilieleza kuwa wanatambua na kuthamini mchango wa tiba asili kutoka Afrika, na kwamba dawa hizo pia zinapaswa kupewa nafasi sawa katika kufanyiwa majaribio kama dawa kutoka maeneo mengine duniani.