Waziri wa Afya Tanzania, Ummy Mwalimu ametoa taarifa kuwa mgonjwa wa virusi vya Covid -19 aliyekuwa mkoani Kagera amepona ugonjwa huo na kufanya jumla ya wagonjwa waliopona kuwa watatu.
Amebainisha kuwa mgonjwa aliyekuwa amebaki mkoani Arusha, vipimo vyake kwa siku ya tisa sasa vimeonesha hasi yaani amepona lakini wizara itaendelea kumpima hadi zitakapofika siku 14 ili kujiridhisha kama anaweza kurejea nyumbani.
Hata hivyo Ummy amesema kuwa wagonjwa wengine 15 wanaendelea vizuri, na hakuna kisa kipya cha mgonjwa wa covid – 19.
“Mungu ni mwema. Na leo pia hatuna case mpya za COVID19. Mgonjwa wa Kagera (Ngara) amepona. Sasa jumla ya waliopona ni 3. Mgonjwa aliebaki wa Arusha vipimo vyake siku ya 9 leo ni Negative. Tutampima siku ya 14 ili kujiridhisha kama amepona. Wagonjwa wengine 15 waliobaki wanaendelea vizuri.” Ameandika Waziri Ummy kwenye ukurasa wake wa Instagram
Na ametoa shukurani kuwa “Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi kwa kuzingatia maelekezo ya Wataalam wa Afya ili kujikinga na Ugonjwa huu ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka”.
Na kusisitiza wananchi kuongeza nguvu katika kuepuka misongamano, au mikusanyiko pia kuzingatia kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.