Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) imemsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wake, Dkt. Anselm Moshi pamoja na watendaji wengine waandamizi wa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa CPB, Salum Hagan, imesema uamuzi huo ni sehemu ya ahadi za bodi hiyo kuleta mabadiliko na kuboresha huduma na biashara ya nafaka nchini.
“Desemba 30 mwaka 2022, bodi ya wakurugenzi ilikaa na kupitisha azimio la kumsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa taasisi, mkurugenzi wa fedha na utawala, mkurugenzi wa biashara, meneja wa kanda ya mashariki, meneja wa kanda ya ziwa, na meneja wa kanda ya kaskazini,” amesema Hagan.
Amefafanua kuwa uamuzi huo umefanywa baada ya bodi kwa kushauriana na Wizara ya Kilimo kujadiliana tuhuma za ubadhilifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutoonyesha uwezo wa kuivusha bodi kwenda hatua ya mbele zaidi zinazoikabili CPB.
“Bodi itaunda timu maalum ya kufanya uchunguzi zaidi kabla ya uamuzi mwingine haujatolewa,” amesema Hagan kwenye taarifa yake.
Hagana ameongeza kwamba CPB pia imeachana na mfumo wa biashara ya rejareja, imesitisha matumizi ya ofisi za bodi nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) na zile za Sudan Kusini huku ikiandaa mpango mkakati mpya wa masoko na kupunguza urasimu.