Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kanda ya kati – CPB, imenunua mazao yenye thamani ya Shilingi 9.6 Bilioni na kuzalisha Tani 480 zilizotolewa msaada Nchini Malawi na zile za Mkoa wa Iringa ambazo ni Tani 520 na kufanya jumla yake kuwa Tani 1000.
Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma hii leo Aprili 4, 2023 Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kanda ya kati, Lelansi Mwakibibi amesema CPB pia inatarajia kununua tani nyingi zaidi katika msimu wa 2023-2024.
Amesema, “hivi karibuni kama tunavyofahamu Rais wetu Dkt.Samia ametoa msaada wa unga kupeleka Nchi ya Jirani yetu Malawi kiasi cha Tani 1000 na sisi kanda ya kati Mkoa wa Dodoma tumetoa Tani zetu na Mkoa wa Iringa wametoa Tanzi zao.”
Aidha, Mwakibibi ameongeza kuwa, “tunaendelea pia kujenga ushirikiano Mzuri kwa baadhi ya Nchi jirani ili kuendelea kukuza biashara ya Mazao Bora zaidi hili ni suala la kujivunia kwetu.”
Ameongeza kuwa, CPB inajivua kutengeneza Soko la wakulima na Wafanya biashara hususani katika zao la Mahindi, Mtama, Alizeti, Mafuta ghafi, Mchele, Maharage pamoja na Nafaka nyingine nyingi.
Kwa upande wake, Afisa masoko Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Kanda ya kati Mkoa wa Dodoma, Tumpe manongi amesema kanda ya kati ina Viwanda viwili ambapo kimoja ni cha kuchakata mahindi Tani 60 na kuzalisha unga Tani 47 Kwa Siku.
Amesema, “Kiwanda cha kwanza kinauwezo wa kuchakata Mahindi Tani 60 kwa Siku na kuzalisha Unga Tani 47 kwa siku na huku kingine ni kiwanda cha kukamua alizeti chenye uwezo wa kukamua Tani 40 kwa siku.”