Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), inatarajia kuwakutanisha makandarasi na wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi mkoani Dodoma Ili kujadili mchango wa Makandarasi katika Uchumi wa Tanzania.
Mkutano huo wa siku mbili wa mashauriano utafanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center mkoani Dodoma kuanzia May 12 2022 hadi May 13 mwezi huu.
Msajili wa Bodi , Mhandisi Rhoben Nkori Amesema kuwa mkutano huo utawashirikisha wadau wote wakiwemo waajiri, wataalamu washauri, wahandisi na wabunifu majengo.
Aidha wengine watakaoshiriki ni wakadiriaji majenzi, watunga sera za uwezeshaji wananchi kiuchumi na wataalamu mbalimbali katika sekta ya ujenzi na kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Umuhimu na Mchango wa Makandarasi katika uchumi wa Tanzania’.
“Mkutano huu wa mashauriano ambao unafanyika kila mwaka ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya ujenzi kwa ujumla wake. Wataalamu wa sekta mbalimbali wanakaribishwa kujisajili mapema ili washiriki katika mkutano,” Amesema Mhandisi Nkori
Hata hivyo, ametaja mada zitakazotolewa kwenye mkutano huo ni pamoja na mchango wa makandarasi katika uchumi wa Tanzania na changamoto zinazoathiri mchango wa makandarasi katika uchumi wa nchi, mada nyingine ni masuala ya kodi ya kuzingatiwa kwa makandarasi ili kuboresha mchango wao katika uchumi wa taifa na fursa katika sheria na kanuni za manunuzi ya umma kuwezesha mchango wa makandarasi wa ndani.
Sambamba na hayo Mhandisi Nkori ametoa wito kwa mashirika na makampuni mbalimbali binafsi na ya umma kwenda kuonesha teknolojia, bidhaa, vifaa na zana za ujenzi.