Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin anaamini kama ratiba ya Ligi Kuu ingetoa nafasi kwa kikosi chake, tofauti na ilivyo sasa, kulikua na uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri zaidi na ikiwezekana wangekuwa kileleni mwa msimamo.

Pablo amesema maneno hayo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, kuelekea mchezo wa kesho Jumatano (Mei 11), ambapo Simba SC itakua mwenyeji wa Kagera Sugar, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha huyo amesema ratiba ya Ligi Kuu imekua ngumu sana kwenye kikosi chake, kutokana na kucheza kila baada ya siku tatu ama nne, jambo ambalo ni gumu na zito kwa wachezaji wake.

Amesema kuna mambo mengi ambayo yalipaswa kuzingatiwa wakati wa upangaji wa ratiba inayoihusu Simba SC hasa baada ya kutoka kwenye michuano ya Kimataifa, lakini imekua tofauti, na ndio maana mambo yanaendelea kuwa mazito kwa wachezaji na hata Benchi la Ufundi.

Kocha huyo kutoka nchini Hispania ametolewa mfano wa ratiba inayowakabili kwa sasa kwa kuigusa Young Africans ambayo kwa siku za karibuni imeonja changamoto hiyo na kujikuta ikiangusha alama sita, kufuatia matokeo ya sare tatu mfululizo.

“Inaonekana hata tukifanya kazi yetu, mtu mwingine atafanya jambo fulani ili isiwezekane. Ukweli wa hali ilivyo ni kwamba tangu Yanga waanze kucheza kila baada ya siku tatu, nne wanazidi kudondosha pointi.”

“Tulipoteza pointi tu katika ligi hii tulipocheza baada ya kila siku tatu mfululizo, tukisafiri bila muda wa kujiandaa na michezo. Watu wanafikiri wachezaji au makocha ni roboti na tunaweza kucheza wakati wowote. Hata kwa wachezaji wa Ulaya haiwezekani kucheza kila siku tatu.”

“Na sasa timu ambayo ulidhani ni bora kuliko sisi lakini hawaoneshi wakati wana ratiba sawa na sisi, na wana dondosha pointi nyingi zaidi.”

“Ndiyo maana huwa nasema kwa ratiba ya haki kwa timu zote mbili na maamuzi ya haki kutoka kwa mambo ambayo hatuwezi kudhibiti labda tungekuwa kileleni.”

Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 46, imekua ikicheza kila baada ya siku tatu ama nne, tangu ilipotolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

CRB kuwakutanisha wadau wa sekta ya ujenzi Dodoma
Haji Manara awavaa Waandishi wa Habari, Wachambuzi