Benki ya CRDB imemuunga mkono Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwenye kampeni ya Ujenzi wa Ofisi za kisasa za Walimu kwa kutoa kiasi cha Shillingi Million 200.
Benki hiyo imeanza kwa kukabidhi hundi ya Shillingi Million 100 leo kati ya 200.
Akipokea hundi hiyo mkuu huyo wa mkoa, Makonda amesema fedha hizo zitasaidia kununua mifuko 20,000 ya Saruji itakayosaidia kufyatua matofali 560,000 ambayo yatajenga ofisi 88 za walimu.
Makonda ameishukuru CRDB kwa kuamua kumuunga mkono kwenye kampeni hiyo ya kuhakikisha walimu wanafanya kazi katika mazingira mazuri yatakayowapa morali ya kufundisha.
“Kazi yangu ni kumsaidia Rais kupunguza au kuondoa changomoto zilizopo ndani ya Mkoa na sio kuwa mzigo kwa Rais, tayari Rais Magufuli ameshatuonyesha njia katika Sekta ya Elimu alipoamua kutoa Elimu Bure kuanzia msingi hadi sekondari kwa lengo la kuwawezesha wanyonge kupata elimu, kwa tendo hilo limetupelekea sisi wasaidizi wake kuona tuna wajibu wa kutatua changamoto kwenye sekta ya elimu”. Amesema Makonda
Makonda amesema imekuwa ni ndoto yake kuona Walimu anathaminika ndio maana aliwapambania wasafiri bure kwenye Daladala na Treni na sasa amehamia kwenye ujenzi wa ofisi za walimu.
Naye Mkurugenzi wa Bank ya hiyo, Dkt. Charles Kimei amempongeza Makonda kwa kuwa mbunifu na mwenye mawazo chanya ya kuwasaidia wananchi hususani wanyonge na kueleza kuwa wataendelea kumuunga kwenye kila jambo kwakuwa kila fedha wanayoitoa inafanya kazi iliyokusudiwa.