Klabu ya Crystal Palace imepata ushidi wake wa kwanza katika ligi kuu ya Uingereza baada ya kuwachapa mabigwa watetezi Chelsea kwa mabao 2-1.
Huu ni ushindi wa kwanza kwa kocha Roy Hodgson tangu alipojiunga na klabu hiyo akichukua nafasi ya Frank de Boer aliyetimuliwa na klabu hiyo baada ya kufungwa michezo minne mfurulizo.
Palace walitangulia kupata bao dakika ya 11 baada ya beki wa Chelsea Cesar Azpilicueta kujifunga lakini dakika nane badae Chelsea walisawazisha bao hilo baada ya Tiemoue Bakayoko kuunganisha kona iliyopigwa na Fabregas.
Wilfried Zaha akiwa amerudi baada ya kuuguza jeraha aliweza kufunga bao la pili kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza na mpaka dakika tisini zinamalizika kikosi hicho cha Hodgson kiliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Hatahivyo ushindi huo hautaiondoa Crystal Palace katika mkiani mwa ligi kuu kwani wamepata pointi tatu tu katika michezo nane waliyocheza mpaka sasa.
Chelsea wanabaki katika nafasi ya nne wakiwa sasa wako na pointi tisa nyuma ya Manchester City ambao wanaongoza msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 22.