Chama cha Wananchi (CUF) kimeweka wazi kuwa hakikubaliani na wazo alilotoa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema, Hashim Juma kuhusu kumpa nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad kugombea Urais.
Juma alitoa wazo kuwa endapo CUF itaendelea kuwa na mgogoro hadi mwaka 2020, Chadema itamkaribisha Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, kugombea Urais wa Zanzibar akiwa na wabunge wake wote.
Akijibu kauli hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmad Mazrui amesema kuwa suala hilo halipo kwani chama chao kinaendelea kujiimarisha na kinakwenda vizuri.
“Chama chetu kitasimama tena upya na kitaweza kukabiliana na chaguzi zozote zitakazojitokeza nchini, suala la kuhama na kuhamia Chadema katika chama chetu hakuna,” Mtanzania linamkariri Mazrui.
Alisema kuwa misukosuko wanayopitia viongozi wa CUF na chama chao tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, imekifanya kuwa imara zaidi na kwamba anaamini itakwisha punde.
Mazurui amewataka Wazanzibar kutozifuatilia kauli za kuhamia Chadema kwani nia ya CUF ni kuwaletea maendeleo na kuwakomboa kiuchumi.
Kauli ya mzee Juma ilizua mjadala na kusababisha Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji kutoa tamko lake, ambapo alisema hayo yalikuwa mawazo ya wazee hivyo watayajadili na hawawezi kuyapuuza.