Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Wananchi CUF, Khalifa Suleiman Khalifa amesema katika kipindi cha uongozi wake atahitaji kushirikiana kwa karibu na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ili kutimiza majukumu yake.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio, ambapo amesema katika kuhakikisha CUF mpya inazaliwa atahakikisha anashirikiana na baadhi ya viongozi wenzake wa vyama vya upinzani pamoja na Chama Cha Mapinduzi CCM.
Amesema kuwa akikutana na kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) atamwambia kuwa chama ni taasisi ambayo inadhamira ya kujenga nchi, hivyo atamuomba ushirikiano ili kuweza kupata mafanikio ya vyama.
“Ninaposema ushirikiano sisemi mimi nitachukua ilani yao nikaitekeleza, napokutana na Bashiru kwanini nigombane naye nikitengeneza ugomvi na Bashiru nitafaidika nini yeye ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala sasa usipozungumza vizuri na viongozi wa CCM, unadhani utafanya mkutano wa hadhara,”amesema Khalifa Suleiman.
Hata hivyo, Khalifa Suleimani ni Katibu Mkuu wa pili tangu kuanzishwa kwa Chama Cha Wananchi CUF, ambaye amerithi nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alitangaza kuhamia Chama Cha ACT-Wazalendo baada ya mgogoro wa kiuongozi uliodumu kwa zaidi ya miaka 3.