Wafanyabiashara na Wawekezaji kutoka Jamhuri ya Czech wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa Pamba pamoja na viwanda vya nguo hapa nchini.
Akielezea kuhusu wafanyabiashara hao kuwekeza hapa nchini waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Miloslav Stasek amesema kuwa wamefurahishwa na mazingira ya biashara huku wakionyesha utayari wa kuwekeza katika sekta ya kilimo na viwanda.
Waziri Stasek ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi leo Oktoba 8, 2021 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni moja ya ziara yake ya kikazi hapa nchini.
Aidha Waziri Stasek amesema majadiliano na uongozi wa TIC umefungua fursa na kutambua masuala mbalimbali yatakayosaidia kuongeza ushirikiano na kuimarisha sekta ya uwekezaji kati ya Czech na Tanzania kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Mimi na Timu yangu tumejadili mambo mbalimbali ya kuwekeza hapa Tanzania ikiwa ni pamoja na utengezaji wa ndege, kilimo, teknolojia pamoja na viwanda,”
“Moja ya kampuni niliyoambatana nayo inauzoefu mkubwa katika uzalisha dawa na vifaa tiba, hivyo kampuni hii itakapo pata fursa ya kuwekeza hapa Tanzania itasaidia kuimarisha mahusiano yetu pamoja na kuboresha sekta ya afya,” Amesema Waziri Staŝek.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa mara baada ya mazungumzo ya awali, wawekezaji hao wameonsha nia kubwa sana ya kuwekeza katika Pamba na viwanda vya nguo hapa nchini.
“Wameonesha uwezo mkubwa katika biashara na uwekezaji kwenye maeneo ya ufundi wa ndege ambapo baadae kutakuwa na mafunzo mbalimbali ya kubadilishana ujuzi na uwekezaji………lakini pia wamevutiwa na sekta ya kilimo hasa katika viwanda vya kutengeneza mafuta ya kula,” Amesema Dkt. Kazi.
Nae Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunatangaza fursa za biashara na uwekezaji.