Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Poland Czeslaw Michniewicz amethibitishiwa hataongezwa Mkataba mpya wa kuendelea na kazi yake, na mwishoni mwa mwezi huu ataondoka rasmi.
Chama cha Soka nchini Poland ‘PZPN’ kimefikia makubaliano na Kocha huyo, baada ya kushindwa kufikia lengo la kuifikisha mbali Timu ya Taifa katika Fainali za Kombe la Dunia.
“Baada ya kikao cha muda mrefu na Kocha Michniewicz, tumekubaliana kuwa hatutamuongezea mkataba, hivyo mwishoni mwa mwezi huu ataondoka rasmi kufuatia mkataba wake kumalizika,” imeeleza taarifa ya PZPN
Michniewicz mwenye umri wa miaka 52, alianza kazi ya kukinoa kikosi cha Poland Januari 2022 akichukua nafasi ya Paulo Sousa, aliyetimuliwa Desemba 2021.
Poland ilianza kamepni ya Fainali hizo kwa kulazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Mexico, kisha ikaifunga Saudi Arabia 2-0 na baadae ilipoteza 2-0 dhidi ya Mabingwa Argentina.
Katika hatua ya 16 Bora Poland ilipoteza dhidi ya Ufaransa na kutupwa nje rasmi ya Faianli hizo, zilizofikia tamati Jumapili (Desemba 18).