Diamond Platinumz ameanika kiasi cha fedha alichoombwa na rapa wa Marekani, Micheal Ray Stevenson maarufu kama Tyga alipotaka kumshirikisha kwenye wimbo wake.
Diamond ambaye anaongoza kwa kufanya ‘collabo’ na wasanii wengi wakubwa wa Marekani akiwemo Omarion, Rick Ross, Morgan Heritage (kundi) ameeleza kuwa huingia gharama kubwa katika kufanikisha kazi hizo ikiwa ni jitihada za kuutangaza muziki wa Tanzania kwenye anga za kimataifa.
Ameyasema hayo wiki hii alipokuwa akitoa maoni yake katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wakati wa mkutano kuhusu suala la kugawanywa kwa asilimia za mapato ya nyimbo (hususan miito ya simu)kwa wasanii ili kupata usawa; kwani wote ni wafanyabiashara na wanahitaji kuungwa mkono katika kuutanza muziki wa Tanzania Kimataifa.
Alisema kuwa alipotaka kufanya ‘collabo’ na Tyga anayefanya kazi chini ya lebo ya ‘Young Money’ inayomilikiwa na Lil Wyne, alitakiwa kutoa kiasi cha $150,000 (Sawa na Sh. 345 Milioni za Tanzania).
Collabo ya kwanza ya kimataifa ya Diamond ilikuwa kati yake na msanii wa Nigeria, Davido ambaye kwa mujibu wa Ommy Dimpoz ambaye alidai awali alitaka kufanya kazi na mkali huyo wa ‘Skelewu’ alipokuja kwa mara kwanza Tanzania, alidai kiasi kikubwa cha fedha.
Hata hivyo, ni ‘Number One Remix’ ambayo Diamond aliifanikisha na Davido iliyofungua milango ya kujulikana kimataifa kwa msanii huyo kutoka Tandale.
Mtindo wa kuwalipa wasanii wa Marekani kufanya nao ‘collabo’ sio suala geni kwa wasanii wa Afrika. Mwaka 2017, rapa M.I Abaga wa Nigeria aliweka wazi kuwa alimlipa rapa Nas Escoba kiasi cha $50,000 (Sawa na Sh. 115 Milioni za Tanzania) kwa ajili ya kupata shairi moja tu la rapa huyo ili aliweke kwenye wimbo wake wa ‘Man’.
Hata hivyo, M.I kupitia lebo yake ya Chocolate City walimfungulia kesi rapa huyo wakidai kuwa shairi alilowatumia sio zuri ukilinganisha na uwezo wa Nas wanaoufahamu, hivyo waliiomba Mahakama kumlazimisha kuwatumia shairi lingine au kuwarudishia fedha.
Kesi hiyo bado inaendelea, huku Nas akiitaka Mahakama kutoyakubali maombi ya Chocolate City dhidi yake.