Daktari wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Lisobine Kisongo, amethibitisha kuwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameondolewa katika kikosi cha timu hiyo kitakachoikabili Sudan baadae leo Jumanne (Machi 29) katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki.
Stars itaendelea kuwa nyumbani katika mchezo huo, baada ya kuifumua Jamhuri ya Afrika ya Kati Jumatano (Machi 23), mabao 3-1.
Mtaalam huyo wa tiba, Amesema Feisal alipata jeraha la kuchanika nyama za paja Januari 26 mwaka huu, tangu wakati huo amekuwa akitibiwa lakini baada ya kumfanyia vipimo vya kina, wamebaini bado jeraha hilo halijapona sawasawa
“Tungeweza kuendelea kumtumia lakini kwa maslahi ya yake, klabu yake na Taifa kwa ujumla tumeona ni vyema tukamruhusu ili akatibiwe zaidi,”
“Katika uchunguzi wetu tumegundua Fei Toto aliumia muda mrefu tangu Januari 26, mwaka huu akiwa na klabu yake ya Young Africans, alipokuja Stars alifanyiwa uchunguzi na kubainika ana tatizo, hivyo anatakiwa kufanyiwa matibabu ya kina,” amesema Lisobine Kisongo
Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen ameuzungumzia Mchezo dhidi ya Sudan, kwa kusema kikosi chake kipo tayari kupambana.