Kocha Mkuu wa Biashara United Mara, Vivier Bahati, amesema safu yake ya Ushambuliaji imeonesha kupambana kikamilifu tangu alipoanza kazi klabuni hapo.

Kocha Vivier ambaye aliwahi kufanya kazi Azam FC kama Kocha Msaidizi, aliajiriwa Biashara United Mara akichukua nafasi ya Kocha Patrick Odhiambo aliyeondoka mwanzoni mwa msimu huu.

Kocha Vivier amesema: “Nina washambuliaji wenye uwezo na kipaji katika ufungaji kama Collins Opare na Chriss Zigga hawa wote wamefanya kazi yao vizuri na ndio tegemeo letu katika ufungaji,”

Ameongeza kuwa, kwa sasa ana uhakika kikosi chake katika kila mchezo ulio mbele yao wataondoka na pointi zote tatu, kutokana na makali ya safu yake ya ushambuliaji.

“Kwa sasa katika kila mechi tutakazocheza nina uhakika wa kuweza kuondoka na pointi tatu, hivyo tunaendelea kujifua na kujipanga zaidi ili tuweze kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.”

“Najua kwamba, Ligi ni ngumu, lakini na sisi tunajiona kwamba, tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwa sasa.”

Biashara United Mara ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ikiwa na alama 22, baada ya kucheza michezo 18.

Will Smith ampiga kofi mchekeshaji jukwaani
Di Maria awaaga mashabiki Argentina