Ugumu wa maisha, mkanganyiko wa kifamilia na mahusiano ya kimapenzi ni kati ya sababu nyingi zinazosababisha mtu kuchukua uamuzi wa kujiua.
Je! utamgundua vipi mtu mwenye dalili za kutaka kujiua? Mwanasaikolojia na mhadhiri wa chuo kikuu, Novelt Deogratius amezitaja baadhi ya dalili za kumgundua mtu wa aina hiyo ambapo amesema,
“ Dalili kuu ambazo unaweza kumgundua mtu anayetaka kujiua ni, kwanza kabisa kujitenga sana na watu, mtu kama huyu anapenda sana kukaa peke yake japo kwenye hili sio wote wanaopenda kujitenga wana hatari ya kufikia maamuzi hayo magumu. Kiashiria kingine ni mtu kulizungumzia sana suala la kujiua, mfano mtu hutumia maneno kama ‘natamani kujiua, au mkiskia nimekufa msishangae’ ”.
Dalili nyingine aliyoitaja mwanasaikolojia huyo ni mtu kuandaa mazingira rahisi ya yeye kujiua, ambapo amesema mtu kama huyo hupenda kujiwekea mazingira yake vizuri kama vile kununua sumu, kamba na kuandika waraka wa mwisho atakaouacha baada ya kujiua, japo maandalizi hayo hufanya kwa siri kiasi cha kwamba ni vigumu kuweza kumtambua.
Novelt Deogratius pia amesema kuwa wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kujiua kutokana na kutopenda kuweka wazi sana matatizo na changamoto zao huku wanawake wakiwa wanaongoza kufanya majaribio mengi ya kujiua ambayo hayafanikiwi.