Nyota wa zamani wa Leciester City, Danny Drinkwater amestaafu soka akiwa na umri wa miaka 33 kwa sababu ya kukosa timu ya kuichezea.
Drinkwater alikosa timu ya kukipiga tangu alipotemwa na Chelsea Julai mwaka jana (2022) ndio maana ameamua kustaafu.
“Napenda kutangaza rasmi nimestaafu rasmi soka la kulipwa. Ilikuwa muda mrefu sana hususan mwaka jana, lakini muda umefika wa kutoa taarifa.
“Sidhani kama itanisumbua kusema kwa sababu nimejiandaa nilisubiri sana nipate nafasi ya kucheza lakini haikuwezekana, sikupata kwani thamani yangu bado ipo kwenye soka,” alisema Drinkwater.
Drinkwater alitokea Manchester United kabla ya kutolewa kwa mkopo mara kadhaa kwenye timu za Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kuibukia Leicester mwaka 2016.
Akiwa Leicester alitengeneza jina lake, alipocheza michezo 218 na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka 2016.
Mafanikio ya Drinkwater yalimhakikishia uhamisho wa Pauni 35 milioni, lakini msimu wake wa kwanza Chelsea alikumbwa na majeraha na kucheza mechi 12 za ligi tu.
Drinkwater ambaye aliichezea Timu ya Taifa ya England mara tatu baada ya hapo hakujumishwa katika kikosi cha Chelsea baadae akatolewa kwa mkopo Burnley, Aston Villa, Kasimpa ya Uturuki na hatimaye Reading kabla ya mkataba wake kumalizika Chelsea Juni mwaka jana.
Drinkwater alifichua siri kwamba kabla ya kustaafu alikuwa na matumaini ya kuhamia Saudi Arabia na pia kukiri alikuwa tayari kurejea tena Leicester.