Serikali Nchini, ipo mbioni kupitia na kurekebisha mitaala ya elimu kwa Vyuo Vikuu na vya Kati kwa ajili ya kutengeneza wataalam wa kutosha na wenye ushindani mkubwa kuhudumia Sekta ya Madini nchini.
Kauli hiyo, imetolewa na Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Ruben Lekashingo jijini Dodoma, katika mahojiano maalum na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Madini na kudai kuwa katika kutafsiri Maono 2030 Madini ni Maisha na Utajiri, Wizara ya Madini imeamua kuongeza nguvu katika nyanja ya uboreshaji wa tija kwa watumishi pamoja na watoa huduma katika sekta ya madini.
Amesema, katika kusimamia ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini, Serikali itashirikiana na Kampuni zilizowekeza sekta ya madini hapa nchini ili kujua uhitaji wao kwenye huduma wanazopatiwa na Watanzania katika miradi yao.
“Tunashirikiana na kampuni hizi ili kujua nini wanahitaji, ili tuboreshe mitaala kwenye vyuo vyetu, kuanzia vyuo vikuu hadi vyuo vinavyofundisha wanaotoa huduma, tunataka tuwe na mitaala ya kimataifa ili wakitoka mafunzoni wakatoe huduma stahiki, wapate uzoefu na waelewe kazi kimatendo,” alisema Janet.
Aidha, amesisitiza namna nyingine iliyopangwa ni kuwaangalia Watanzania ambao walifanya kazi hapa nchini na kutoka nje kufanya kazi kama wataalam kwa kupata taarifa zao ili warudi nchini kufanya kazi kwenye kampuni zilizopo kwa lengo la kufundisha Watanzania ujuzi waliojifunza katika nchi tofauti tofauti.
Kamishna Janet aliongeza kuwa lengo la Wizara kufikia 2030 ni kuhakikisha huduma stahiki inatolewa kwa maboresho ili kuongeza tija kupitia wataalam wa ndani na nje ya nchi kwa watumishi na wafanyakazi kwenda nje kujifunza au kuleta wataalam kuja kuwafundisha wafanyakazi hapa nchini.
Katika kikao cha Wachimbaji Wakubwa na Wadogo kilichofanyika Oktoba 27, 2023 jijini Dar es Salaam, Kamishna Janet alidokeza mambo kadhaa ambayo Serikali imepanga ikiwa ni maandalizi ya Tanzania kuhakikisha inashiriki ipasavyo katika uchumi wa Madini Mkakati na Muhimu.