Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi zimefanya mkutano wao ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu uliowekwa na Wizara kukutana na Wachimbaji Wakubwa, wa Kati na Watoa huduma migodini kila robo ya Mwaka, kupitia Chemba ya Migodi.

Akizungumza katika mahojiano, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mikutano hiyo inatumika kama njia ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa miradi wanayoisimamia ili kuchochea uwekezaji.

Amesema, ‘’tukiondoa vikwazo itasaidia kuongeza shughuli za uchimbaji nchini na hatimaye tutaongeza uchumi na mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, tutaongeza ajira, maendeleo ya nchi na watu. Chukulia mfano wa Mkoa wa Geita tu, Serikali inakusanya shilingi bilioni 243, tunataka shughuli za madini zifanyike mikoa yote katika mazingira rafiki.’’

Mavunde ameongeza kuwa, “kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania – GST, Wizara inalenga kufanya tafiti za kina, ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 kutoka asilimia 16 ya sasa. Tanzania ina utajiri wa kutosha wa madini mkakati na kwa kuzingatia mahitaji ya dunia ya tani milioni 150 ya madini hayo ifikapo mwaka 2050, ni lazima ijipange kunufaika kiuchumi,’’ amesema Mavunde.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi, Mhandisi Philbert Rweyemamu amesema kuwa lengo la mikutano hiyo ni kujadili na kujenga uelewa wa pamoja katika masuala mbalimbali hususan masuala yanayohusu mifumo ya Kisheria na Kisera na kuongeza kwamba, mikutano hiyo inalenga kuiwezesha sekta ya madini kuendelea kufanya vizuri.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesema utaratibu huu unawezesha serikali kupata mrejesho na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na wadau na kueleza kuwa, lengo la serikali ni kuwawezesha wadau kutekeleza majukumu yao vizuri kupata faida na serikali kunufaika kupitia rasilimali madini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau wamepongeza utaratibu wa kukutana na kujadili kwa pamoja na baadhi kupendekeza taasisi nyingine za umma zinazohusika na masuala ya madini moja kwamoja kushirikishwa katika mikutano hiyo, ili kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya madini.

Mkutano huo, ni wa Pili kufanyika baada ya mkutano wa kwanza uliofanyika mapema mwezi Julai, 2023, yote ikilenga kuleta ukaribu kati ya serikali na wadau wa sekta ya madini pamoja na kujadili kwa pamoja changamoto ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia utekelezaji wa miradi, shughuli na biashara ya madini nchini.

Waacheni Wafanyabiashara wafanye kazi - Dkt. Kijaji
Balozi, Profesa wapanga kuimarisha usalama wa kikanda